Ubatizo: je, nini tofauti ya ubatizo wa maji na wa Roho Mtakatifu?.
Kuna imani na mafundisho mengi yanayohusiana na ubatizo, na tumejifunza kwamba ubatizo ulianza kuonekana katika vitendo wakati wa mwanzo kabisa wa Agano Jipya. Kulingana na Maandiko, Yohana Mbatizaji alipewa ujumbe wa kwanza wa ubatizo, ambao ulikuwa ubatizo wa Maji. Yeye alikuwa mtangulizi katika huduma kabla ya Yesu Kristo. Yohana alikuwa akibatiza watu katika maji ya mto Yordani. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba ubatizo haukuanza na Yesu Kristo, kwani kulikuwa na watu wengine waliobatizwa kabla yake.Kuna maswali kadhaa yanayojitokeza katika suala la ubatizo kutokana na majibu aliyoyatoa Yohana Mbatizaji kwa watu waliomuuliza kuhusu ubatizo. Aidha, maneno ya Yesu mwenyewe juu ya ubatizo ni muhimu kuzingatiwa, hasa aliposema hayo baada ya kubatizwa kwa ubatizo wa Maji.

Majibu ya Yohanajuu ya ubatizo alioufanya .
Kuna utata unaosababishwa na majibu ya Yohana Mbatizaji kwa sababu watu mbalimbali, kama wasomi, viongozi wa serikali, waandishi, na viongozi wa dini, walimfuata na kumuuliza ikiwa yeye ndiye Kristo. Walikuwa wamesoma katika vitabu vya manabii wa kale wa Israeli kwamba Kristo atakapokuja, ndiye atakayebatiza. Walipoona Yohana akibatiza watu, walimwendea na kumuuliza ikiwa yeye ndiye yule aliyetabiriwa kuwa Kristo. Hata hivyo, Yohana aliwajibu akisema, “Mimi siye.” Wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, kwa nini basi wabatiza?” Yohana akawajibu akisema, “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba, lakini yupo yule ajaye nyuma yangu, ambaye alipaswa kuwa mbele yangu, atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”
Yohana alikuwa anafanya ubatizo kwa ajili ya toba. Watu walimwendea ili kuungama na kutubu dhambi zao, na kisha akawabatiza katika maji. Hivyo, wakati wa Yohana, watu wa Israeli walirejea katika Maandiko na kuona kwamba ilikuwa imetabiriwa kwamba Masihi atakapokuja, moja ya mambo atakayofanya ni kubatiza. Mambo mengine ambayo Masihi alitarajiwa kuyafanya ni pamoja na kuikomboa Israeli kutoka utumwani na kuwaokoa watu kutoka katika dhambi zao. Rejea.. Marko 3: 1 – 8. Mathayo 3: 1 – 17. Huo ndio ubatizo wa Maji wa Yohana kwa ajili ya toba kwa Israeli.
Maswali ya Ubatizo wa Yohana.
Katika suala la ubatizo, Yohana mwenyewe alieleza kwamba yupo Mkuu zaidi ya yeye ambaye atawabatiza watu kwa Roho Mtakatifu. Hii inamaanisha kuwa ubatizo wa Yohana kwa maji ulikuwa ni kielelezo na maandalizi ya ubatizo ujao ambao ungefanywa na Yesu Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, kwa sasa, tunapaswa kufuata ubatizo ulioanzishwa na Yesu Kristo ambao ni ubatizo kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Yohana alikuja kuandaa njia kwa ajili ya Yesu Kristo na kumtangaza kama Masihi aliyekuja kuwaokoa watu kutoka katika dhambi zao. Hivyo, baada ya Yesu kufanya kazi yake ya ukombozi, tunapaswa kufuata mafundisho na maagizo ya Yesu Kristo kuhusu ubatizo wa kimaanawi kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ubatizo wa maji wa Yohana ulikuwa ni ishara ya kutubu na kujiandaa kwa kuwapokea Masihi.
Hata hivyo, mara Yesu alipofika duniani na kutekeleza kazi yake ya ukombozi, mfumo wa ubatizo ulibadilika. Baada ya ufufuo wake, Yesu aliagiza wanafunzi wake kubatiza watu kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.

Ubatizo wa Yohana kwa Yesu Kristo.
Ni kweli, ubatizo wa Yesu ulikuwa wa kipekee na uliambatana na matukio muhimu. Yohana alimwambia wazi kuwa yeye si mwenye sifa za kulegeza gidamu za viatu vyake, na kwamba yupo Mkuu zaidi ya yeye ambaye atawabatiza watu kwa Roho Mtakatifu na moto. Wakati Yesu alipokuja kubatizwa na Yohana, Yohana alipata ufunuo kutoka kwa Mungu kwamba atakayemwona Roho akishuka na kukaa juu yake ndiye Masihi. Kwa hiyo, Yohana alimtambua Yesu kuwa Masihi alipomwona Roho akishuka juu yake kama hua.
Ubatizo wa Yesu ulikuwa ni tofauti na watu wengine kwani uliambatana na kushuka kwa Roho Mtakatifu juu yake. Baada ya kubatizwa, Yesu aliongozwa na Roho hadi jangwani ambapo alijaribiwa na Ibilisi kwa siku arobaini. Hivyo, ubatizo wa Yesu ulikuwa ni tukio muhimu ambapo alitambuliwa kama Masihi na alipokea ungamo wa Roho Mtakatifu. Kabla ya ubatizo wa Yesu, hatujasoma juu ya mtu mwingine akipitia aina hizi mbili za ubatizo, yaani ubatizo wa maji na ubatizo wa Roho Mtakatifu. Ubatizo wa Yesu ulikuwa ni mwanzo wa aina mpya ya ubatizo, ambao unahusisha ubatizo wa maji kama ishara ya kutubu na kujiandaa, pamoja na ubatizo wa Roho Mtakatifu ambao ni kazi ya Mungu katika kumjaza na kumtuma mtu kwa huduma. Baada ya ubatizo wa Yesu, tunao mfano na mwongozo wa kufuata katika ubatizo wa kimaanawi kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
Maneno ya Yesu juu ya Ubatizo.
Yesu anasema katika kitabu cha Marko 10:38, “Hamjui- muliombalo, je, mwaweza kukinywea kikombe nikinyweacho au ubatizo nibatizwao mwaweza kubatizwa?” Hii inamaanisha kwamba Yesu anawauliza wanafunzi wake ikiwa wanaweza kushiriki katika mateso na majaribu ambayo yeye mwenyewe angekabiliana nayo. Anatumia mfano wa kikombe anachokunywa na ubatizo anaopaswa kubatizwa kuelezea dhiki ambayo atapitia. Maneno haya ya Yesu yanasisitiza umuhimu wa kufahamu gharama ya kufuata njia yake. Anaonyesha kuwa kuwa mwanafunzi wake kunahitaji ujasiri na kujitolea kamili. Anaweka wazi kuwa kufuata njia yake kunaweza kusababisha mateso na dhiki, lakini pia inaleta wokovu na uzima wa milele. Hivyo, Yesu anasisitiza umuhimu wa kujitolea kabisa na kuwa tayari kukabili changamoto…
na mateso kwa ajili ya imani yake. Anataka wafuasi wake wawe tayari kubatizwa katika majaribu na kushiriki katika mateso yake, ili waweze kushiriki pia katika uzima wa milele na utukufu wake.

Maswali ya Ubatizo wa Yesu.
Kama Yesu alibatizwa katika Maji na kisha Roho Mtakatifu akamshukia, Je, na sisi tunaofuata Imani katika Yesu Kristo, imetusa kubatizwa katika Maji ndipo Roho Mtakatifu atushukie?
Katika maandiko hayo unaweza ukapata maswali mengi sana kwamba ubatizo wa Yesu aliokuwa akiulenga ni upi?. Je, ni ule wa Yohana.?
Je, nitajuaje kwamba Roho Mtakatifu amenishukia pasipo ishara yeyote kama ambavyo ilitokea kwa Yesu Kristo?
Kama ubatizo wa Maji ni sahihi Je, kwa nini Yesu hakuwahi kubatiza Mtu hata mmoja?
Kama Ubatizo wa Maji sio sahihi Je, kwa nini Yesu aliwwacha wanafunzi wake waendelee kubatiza watu?
Yesu mwenyewe anamwambia Nikodemu kwamba Mtu asipozaliwa kwa Maji na kwa Roho, hawezi kuurithi ufalme wa Mungu, Je, nawezaje kuzaliwa katika Maji na Roho?.
Kama ni ubatizo wa Maji na Roho Mtakatifu kama ambavyo ilitokea kwa Yesu Kristo, Je, napaswa kupata ubatizo wa Maji na Roho kwa mtindo gani?
Ubatizo katika Kanisa la kwanza la Mitume.
Kwa kutambua kwamba yatakuja mafundisho yenye mashaka juu ya ubatizo, Yesu alipokwisha kufufuka aliwaagiza wanafunzi wake akisema. “Enedeni ulimwenguni kote, Mkawafanye Mataifa Kuwa Wanafunzi wangu, Mkiwabatiza, Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Kwa maelekezo haya tunaona dhahiri kwamba Sgizo kuu la Yesu kwa wanafunzi wake ambao ndio Mitume 12 tunaowasoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume, lilikuwa Kuihubiri Injili kwa mataifa yote kwa kuwabatiza Ubatizo aliowaamuru. Hivyo tunaona kwamba Ubatizo ni agizo la Msingi wa Imani kwa Yesu Kristo na ni hatua ya kwanza kuendea Wookovu.
Rejea Mathayo 28:18 – 20. 
Majibu ya Maswali yaliyotangulia.
Ubatizo wa maji wa Yohana ulikuwa kwa ajili ya toba, ubatizo wa Yohana Uliandamana na Maungamo ya dhambi, sio kujazwa Roho Mtakatifu. Bali ubatizo wa Yesu Kristo ni ule unaoambatana na kujazwa Roho Mtakatifu, Swali linalobaki ni Je, baada ya ubatizo wa Maji, nawezaje kujazwa Roho Mtakatifu?, Jibu lake tunalipata Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 19: 1 – 7. Ili kupata uelewa Mkubwa zaidi soma Kitabu chote cha Matendo ya Mitume, na utapata namna ambavyo Mitume wa lanisa la kwanza walitekeleza amri hiyo ya Ubatizo.
Kwa habari ya ubatizo ni dhahiri kwamba tunaweza tukajifunza kwa Mitume kwa kile walichokuwa wakikienzi na kutenda baada ya Yesu kukufuka na Kupaa kwenda mawinguni. Katika kitabu hicho cha Matendo ya Mitume, tunaona ni kwa namna gani ujumbe wa Yesu Kristo ulikuwa ukienezwa kwa njia ya Mahubiri ya Mitume walioachwa na Yesu Kristo. Kwa maono na mapendekezo yangu nadhani ni vyema pia waalimu na wahubiri wa nyakati za sasa, kuanza kuwafundisha waamini wapya wa imani ya Yesu Kristo kwa kuanzia kitabu cha Matendo ya Mitume.
Hitimisho.
katika Maandiko tunafundishwa kwamba Yesu alitengeneza imani moja, ubatizo mmoja kwa Mungu mmoja. Tunaposungumzia ubatizo wa Yesu Kristo, tunarejelea ubatizo aliowakabidhi mitume wake na kuwaagiza jinsi ya kubatiza.
Katika barua ya Mtume Paulo kwa Waefeso, sura ya 4, mstari wa 5 hadi 6, tunasoma hivi: “Mungu ni mmoja, na mnatumaini mmoja; mmetiwa ubatizo mmoja, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zenu; mnayo imani moja, na kuna Roho mmoja, kama ilivyohesabiwa kuwa mmoja tumaini lenu, kwa kuwa kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, aliye juu ya wote na katika wote.” Hapa, Paulo anasisitiza umoja wa imani, ubatizo, na tumaini katika jamii ya waamini. Ubatizo huo ulitolewa kwa ajili ya ondoleo la dhambi, na ni njia ya kuunganishwa na jumuiya ya waamini. Ni kielelezo cha kuungana na Kristo katika kifo chake na kufufuka kwake.
Ubatizo unaashiria kujitoa kwa mtu kwa Yesu Kristo na kuingizwa katika mwili wake, yaani Kanisa. Ni ishara ya kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Ubatizo huo unatuunganisha katika umoja na Wakristo wengine, na sisi sote tunakuwa watoto wa Mungu mmoja na tunaunganishwa katika familia moja ya kiroho. Kwa hiyo, mafundisho haya ya Paulo yanathibitisha umuhimu wa ubatizo na umoja wa imani kwa wote wanaomfuata Yesu Kristo. Ubatizo wetu unatuunganisha katika jumuiya ya waamini na tunapokea Roho Mtakatifu, ambaye anatusaidia kukua katika imani na kutembea katika njia ya Yesu.