Maandiko: Maandiko pasipo ufunuo ni mauti.
MIONGOZO YA MAANDIKO.
Kuna maneno mengi katika Maandiko Matakatifu ambayo yanaweza kuwafanya watu wapate tahayari kidogo wanaposoma, kwa sababu ya kutokuyafasiri ipasavyo. Watu wengi hawasomi Biblia mara kwa mara, na hata wale wanaosoma mara kwa mara mara nyingi wanazingatia kusoma sehemu zilizopendekezwa na waalimu au viongozi wao wa dini. Kusoma Biblia peke yake hakuwezi kukupa uhakika wa kumjua Mungu, lakini kinachoweza kukupatia ni uelewa wa habari za Mungu na wanadamu katika nyakati mbalimbali tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuumbwa kwa Adamu.

Kusoma Biblia kunahusisha maneno mengi ya kinabii na kitaaluma, ambayo yanahitaji ufahamu wa kiroho ili kuyaelewa ipasavyo.
Roho Mtakatifu ndiye anayeweza kutufunulia maana halisi ya maneno hayo, kwani yeye ni mwalimu mwenye uwezo wa kufunua ukweli wa Mungu ulio ndani yetu. Ni sawa kuwa na mwalimu au mchungaji anayetusaidia katika kusoma Biblia, lakini ni muhimu pia kuwa na Roho Mtakatifu ambaye atatufunulia mafumbo yaliyomo ndani ya kitabu hicho. Mwalimu wa Biblia naye pia anapaswa kuwa na Roho Mtakatifu ndani yake ili aweze kutoa mafundisho na miongozo sahihi kwa watu. Biblia bila ufunuo wa Mungu inakuwa kama kitabu cha kumbukumbu za kale au utabiri wa kinajimu, ambapo hata watu wa kawaida wanaweza kutoa tafsiri zao za mambo yaliyofichwa kwa njia ya fumbo. Hivyo, ni muhimu sana kumwomba Roho Mtakatifu atuongoze tunapoisoma au kujifunza Biblia.
Maandiko katika Biblia yalikuwa maneno yaliyotolewa na Mungu kupitia watumishi wake, waliyoyasema chini ya uongozi na mwongozo wa Roho Mtakatifu. Hivyo, ni muhimu sana kusoma Biblia tukiwa tumeungamanishwa na Roho Mtakatifu huyo huyo wa Mungu. Kusoma Biblia si kosa, lakini ni kosa kuitafsiri kwa mujibu wa mapendeleo yetu wenyewe, kwani kuna maneno ya unabii ambayo ikiwa tutayabadilisha na kutoa tafsiri isiyokuwa sahihi, tunajitwisha laana kwa kile tunachosema. Hivyo, ni bora zaidi kunyamaza kuliko kujaribu kuweka maneno na tafsiri zetu binafsi kwa ajili ya maslahi yetu au kwa sababu ya kutokuwa na ufahamu wa kutosha.
Maandiko bila ufunuo ni mauti.
Luka 24: 44-49 Yesu aliwafunulia wanafunzi wake ufahamu wa maandiko ili waweze kuyaelewa. Hii inaonyesha kuwa wanafunzi walikuwa wanafahamu maandiko, lakini walihitaji ufunuo wa ziada. Baada ya kufufuka kwake, Yesu aliwatokea wanafunzi wake na moja ya mambo aliyofanya ilikuwa kuwapa ufunuo juu ya maandiko, ili waweze kuyaelewa kupitia Roho ya Ufunuo.
Wakati tunasoma maandiko bila ufunuo, tunakumbushwa kuwa “maandiko yanaua.” Hata hivyo, tunaposoma kwa ufunuo, “Roho huwapa uzima.” Kwa hiyo, ninaposema katika uchambuzi wangu, siyo kwamba nimefikiria peke yangu, bali Roho aliyeinua mtumishi wake (ABDALAH MOHAMED KALUNDE), na mimi niliyeandika kitabu hiki nilipokea mafundisho kutoka kwake. Alikuwa akinifundisha na kunishuhudia nguvu na ukweli wa Yesu Kristo, na kwa idhini ya Mungu, niliandika ujumbe huu. Kwa hakika, hizi ni ushuhuda wenye nguvu na maisha ya kweli ambayo tulishiriki kwa msaada wa Yesu Kristo kupitia mtumishi wake, Kalunde.

Baadhi ya miongozo ya kukusaidia kusoma maandiko.
Biblia inasema “Yeye asomaye na afahamu”, hii inamaanisha kuwa tunapaswa kusoma na kuelewa kile tunachosoma, iwe ni maarifa ya kiroho au ya kidunia. Ili kupata ufahamu uliokusudiwa, ni muhimu kuelewa kile tunachosoma na kuthibitisha ukweli wake. Biblia ni maandiko yaliyoongozwa na Roho ili tuweze kuyaelewa, na hivyo tunapaswa kuongozwa na Roho Mtakatifu katika kuelewa na kutafakari maandiko hayo. Hatupaswi kuyatafsiri kwa mapendeleo yetu wenyewe.
Mtume Paulo aliandika, “Je, mambo yaliyoandikwa kuhusu wanyama yaliandikwa kwa ajili ya hao wanyama? La hasha, hayakuandikwa kwa ajili ya hao wanyama, bali kwa ajili yetu sisi” (1 Wakorintho 9:9). Hii inaonyesha kwamba maandiko hayo yana ujumbe na maana ambayo yanatuongoza sisi kama binadamu. Waraka huu sio matokeo ya maarifa ya kibinadamu au mapenzi ya mtu binafsi, bali ni kazi ya Mungu katika maisha yetu kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu.
NOTE Mungu aliposema juu ya wanyama, mimea au vitu vingine hakuwa na maana ya vitu hivyo bali alivitumia kama mfano kusudi aweze kumfundisha mwanadamu. Yesu akwaambia makutano akisema ”nimesema nanyi mambo ya duniani hamkunisadiki je, mtanisaidiki vipi nikisema nanyi mambo ya mbinguni?” Andiko jingine linasema “wala pasipo mfano Yesu hakunena jambo”, kwa maana hiyo yapo mambo mengi sana ambayo yalisemwa kwa mifano ila watu wameyapokea kama mambo halisi, jambo ambalo linapoteza shabaha nzuri ya Rohoni na kuendelea kutuhubiria mambo ya mwilini.
katika Biblia, tunasoma kwamba Yesu alitumia mifano kuwasilisha ujumbe kwa watu. Wanafunzi wake walimuuliza kwa nini alitumia mifano wakati wa kuhubiri kwa umati, na Yesu aliwajibu kwamba wao walikuwa wamebahatika kuzijua siri za ufalme wa Mungu, hivyo aliwaeleza waziwazi. Lakini kwa wengine, aliwasilisha ujumbe kwa kutumia mifano ili wasione, wasikie, na wasielewe. Swali muhimu hapa ni: Je, tunapaswa kuendelea kuishi kwa kufuata mifano hiyo? Na ikiwa ndivyo, ni kwa ajili ya akina nani Yesu alitumia mifano? Je, ilikuwa kwa ajili ya wanafunzi wake au umati wa watu? Ni muhimu kuwa waaminifu na watiifu katika kuishi kulingana na mafundisho ya Yesu na kuongozwa na Roho Mtakatifu ili tuweze kufahamu na kuishi kikamilifu kusudi na mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Tafuta hekima na mwongozo wa Mungu katika kila jambo, na endelea kuwa mwanafunzi wa Yesu katika njia yako ya maisha.
Kama tunakiri kuwa wanafunzi wa Yesu, ni muhimu kwetu kuendelea kufuata na kutekeleza mafundisho yake. Siri na mafumbo hayo hayataendelea kuwa siri milele, kwani kupitia mafundisho na mwongozo wa Roho Mtakatifu, tunaweza kuyaelewa na kuyafunua. Hata hivyo, ili kuyatambua na kuelewa makusudi na malengo yaliyomo katika mafundisho hayo, tunapaswa kuwa tayari kuwa na moyo wa kujifunza na kutafuta hekima katika kila jambo. Ishara za kiuanafunzi ni mambo ambayo yanadhihirisha uhusiano wetu na Yesu na jinsi tunavyoishi kulingana na mafundisho yake. Hekima ni mojawapo ya ishara hizo, ambayo inatuongoza kufanya maamuzi sahihi na kuchukua hatua zinazoendana na mapenzi ya Mungu. Maandiko yanasema, “Naye Bwana atawapa akili katika kila jambo” (Luka 21:15). Hivyo, tunapoendelea kusoma makala hii au mafundisho mengine, tunahitaji kumtanguliza Mungu na kumwomba atufunulie akili zetu ili tuweze kuyatambua makusudi na shabaha iliyopo katika fundisho hilo.
Baadhi ya tafsiri ya Ufunuo kutoka katika maandiko.
- Maji ya Mto — Uwepo wa nguvu za Mungu Rohoni mwa Mtumishi.
- Maji ya bahari — Jamii za Mataifa.
- Jangwa — Roho ya Dini ya upotofu.
- Nyika — Roho ya Dini
- Nyoka — Ibilisi.
- Jiwe — Roho ya kiburi.
- Majani mabichi — Neno la utakatifu/Neno la uzima.
- Mti mbichi — Mtumishi wa kweli wa Mungu.
- Mti mkavu — Mtumishi wa uovu.
- Chem chem — Roho Mtakatifu.
- Nchi — Mwili.
- Mbingu — Roho.
- Matope — Maisha ya katikati (Mambo ya Roho na Mambo ya Mwili kwa pamoja).
- Udongo — Mwili.
- Nguruwe — Mtumishi asiyekuwa na Ufunuo wa Mungu.
- Punda — Mtumishi anayefuata mafundisho ya Dini na sio ya Mungu.
- Kambale — Mtumishi asiyekubali Ufunuo.
- Ng’ombe — Mtumishi mwenye maono na Ufunuo.
- Tai — Mfano wa Mungu Baba.
- Vugu vugu — Mtumishi mwenye maisha ya katikati (UOVU NA WEMA).
- Moto — Uwepo wa Roho Mtakatifu.
- Baridi — Kukosa Roho Mtakatifu
- Mkate — Mfano wa matendo ya mwilini.
- Divai — Mfano wa matendo ya Roho.
- Majani makavu — Neno la uovu/Neno la mauti.
Msingi wa maandiko ya biblia.

- Biblia ni kusanyiko la maandiko matakatifu ambayo yameandikwa kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.
- Neno la Mungu linarejelea ufunuo na mapenzi ya Mungu kwa wanadamu, na ni kitu kilicho hai na kinachoweza kuzungumza kwa nguvu na kuleta athari katika maisha yetu.
- Maandiko yanaandikwa na watu.
- Hata hivyo, licha ya mawazo hayo ya kibinadamu, tunasadiki kuwa Maandiko yameongozwa na Roho Mtakatifu na yana ujumbe wa Mungu kwa wanadamu.
- Kuna baadhi ya maneno na majina ambayo yalibuniwa na waandishi wa Biblia, lakini hayo hayapunguzi thamani na ujumbe wa Biblia kwa ujumla.
- Biblia inasema kwamba kuna mambo mengi ambayo Yesu aliyafanya ambayo hayajaandikwa, na hivyo ni dhahiri kuwa yaliyoandikwa ni sehemu iliyochaguliwa ya mambo hayo.
- Ingawa tunatambua kuwa kuna mipaka katika maandiko yaliyoandikwa, tunaamini kwamba Mungu, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ameongoza mchakato wa kuandika na kuchagua maandiko yaliyomo katika Biblia ili kutufunulia mapenzi yake na kusudi lake la wokovu wetu. Rejea Yohana 20:30 – 31.na 1Wakorintho 7;6 na 12/ 1Petro 2:6, 2Petro 1:20, 2Petro 3:16, 1Wakorintho 15:4, Warumi 15:4
Maana ya neno.
Yesu akwaambia “Ninyi mnayachunguza maandiko mkidhania kuna uzima ndani yake, nayo yananishuhudia mimi, nanyi hamtaki kuja kwangu muupate uzima,” Yohana 5:38 – 40. Maandiko hayo yasema wazi wazi kwa habari ya maandiko na Neno la Mungu.na katika Yohana 6:63* tunaona sifa ya neno la Mungu, Neno linapotoka katika kinywa cha Mcha Mungu linatupa uzima. Maandiko yanaweza kupotosha kama yakitumiwa vibaya, kudanganya, kulagai, kulaani, kutoa faraja za uongo, kutoa laana kinyume na makusudi ya Mungu, kama katika makusanyiko ya leo maandiko yanavyotumika kufanya uasi kwa Mungu, kwa kufanya ibada za sanamu. Tumalizie kwa kusoma maandiko haya kama ushahidi wa hatari ya kutegemea maandiko badala ya Roho Mtakatifu. 2Wakorintho 3:6.andiko huua bali Roho huuwisha.
Kugeuza Biblia kuwa kiongozi kwa wacha Mungu, ni kumuondolea nafasi Roho Mtakatifu maishani mwa watu.