Upekee wa Yesu Kristo: Je, asili ya Yesu ni mwanadamu au Mungu?

faith
Author

Benjamini Mpinga

Published

March 1, 2023

Yesu Kristo ni mada muhimu na ya kuvutia kwa watu wengi, kwa sababu yeye ni kiini cha imani ya Ukristo duniani kote. Kuna utata na mjadala miongoni mwa watu kuhusu utambulisho halisi wa Yesu na jinsi ya kumtambua. Baadhi wanaamini kuwa yeye ni Mungu, wengine wanamchukulia kama Nabii wa Mungu, na wengine wanaona yeye kama Mtume wa Mungu.Je, Yesu Kristo ni Mungu au Nabii au Mtume? Katika makala hii tutaangazia baadhi ya matendo na maneno ya Yesu, ili kubaini asili yake na nasaba mahsusi ya kumnasibisha nayo. karibu tuwe sote katika makala hii.

MSINGI WA AGANO JIPYA.

Yesu Kristo alizaliwa katika hali isiyo ya kawaida kabisa, ambayo haitaweza kuelezwa kikamilifu na sayansi ya kibinadamu. Alikuwa amezaliwa na bikira, ambaye hakuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume yeyote, na hakuwa na baba wa kibinadamu. Badala yake, mama yake alipata mimba kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Siku ya kuzaliwa kwake, Wayahudi wote walikuwa wakihesabiwa, na wazazi wake hawakuweza kupata sehemu ya kukaa kwa sababu ya msongamano wa watu katika mji wao. Kwa hiyo, walilazimika kutafuta mahali pa kujifungua, na mwishowe walipata hori la ng’ombe kama mahali pa kujifungulia.

Baada ya kuzaliwa kwake, nyota kubwa ilionekana angani, na wataalamu wa nyota walipotambua ishara hiyo, walielewa kwamba ilikuwa ishara ya kuzaliwa kwa mtu mwenye mamlaka na ukuu. Waliamua kuondoka na kwenda kumwona mtoto huyo ambaye alikuwa amezaliwa na mamlaka ya juu. Habari za kuzaliwa kwa Yesu zilisambaa katika sehemu nyingi za nchi, hata kufikia Mfalme Herode. Aliposikia habari hizo, alishtuka na kuogopa kwamba ufalme wake ungekuwa hatarini, hivyo akatoa amri ya kuwaua watoto wote wachanga wenye umri wa miezi miwili na chini.

Hata hivyo, malaika wa Bwana Mungu alimtokea Yusufu, mume wa Maria na baba wa Yesu, na kumwambia awachukue mama na mtoto na waende Misri, hadi itakapotimizwa amri ya Mfalme, ili mtoto asipate madhara. Yusufu alitii amri hiyo kutoka kwa Bwana Mungu.

Baada ya matukio hayo, tunakuja kumuona Yesu akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, kulingana na desturi ya Kiyahudi, alipelekwa Hekaluni ili atimize matakwa ya Sheria, na baada ya taratibu za ibada zao kumalizika aliketi na wazee kujadiliana mambo ya Mungu, ambapo Yesu alishangaza wazee kwa hekima yake ingawa bado alikuwa kijana mdogo.

Baadaye, Yesu aliendelea kukua kwa umri na maarifa, akimpendeza Mungu na wanadamu, na akisaidia wazazi wake katika majukumu yao ya kila siku. Alipofikisha umri wa miaka thelathini, alibatizwa na Yohana Mbatizaji katika mto Yordani, na kisha aliongozwa na Roho kwenda jangwani kwa ajili ya majaribio. Alibaki jangwani kwa siku arobaini akiwa amefunga, na alijaribi

ISHARA YESU ALIZOZIFANYA KWA VITU.

Yesu alifanya miujiza mingi, jambo ambalo lilikuwa nadra sana kufanywa na Manabii waliotangulia na hata watu/waganga waliokuwa wakiwalaghai wengine kwa ishara mbalimbali. Ishara ya kwanza aliyoifanya Yesu ilikuwa.

kubadilisha maji kuwa divai/mvinyo.

Yesu alibadilisha maji kuwa divai/mvinyo katika sherehe ambapo yeye, mama yake, na wanafunzi wake walihudhuria. Wanafunzi wake na watu wote walioshuhudia tukio hilo walistaajabishwa na ishara hiyo.

Kutuliza mawimbi ya bahari.

Yesu alipokuwa na wanafunzi wake katika mtumbwi, walikumbwa na upepo mkali na mawimbi makali ambayo yalitia hofu ya chombo chao kuzama. Wanafunzi, wakijawa na woga wa kuangamia, wakamwita Yesu. Hapo ndipo Yesu alipoamka na kuukemea upepo na mawimbi hayo, na mara moja yakatulia. Wanafunzi wote waliogopa sana na kushangazwa na ishara hiyo, wakizungumza kwa mshangao, wakisema, “Ni nani huyu ambaye hata pepo na bahari zinamtii?”

Kuulaani mtini nao ukakauka.

Yesu alipokuwa njiani na wanafunzi wake, aliona mti wa mtini ukiwa umechanua majani mabichi. Akiwa na matumaini ya kupata matunda, aliposogelea mti huo, aligundua kwamba haukuwa na matunda. Kwa hiyo, alimlaani mti huo, na mara moja ukakauka. Wanafunzi wake walishangaa sana na wakauliza jinsi jambo hilo lilivyowezekana. Yesu aliwajibu na kuwaambia, “Mkiwa na imani, mtaweza kufanya mambo makubwa zaidi ya haya.”

Kutembea juu ya maji.

SSiku moja, Yesu alikuwa akitoa mahubiri kwa umati mkubwa. Watu walimjia kwa lengo la kumsikiliza, na wengine walileta wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali, wakimtazamia kwa sababu walimwona kama mtu mwenye nguvu na uwezo wa kipekee. Walitaka kumfanya kuwa mfalme wao. Hata hivyo, Yesu aligundua nia zao, na baada ya kumaliza kufundisha na jioni kukaribia, aliwaacha na kwenda ng’ambo ya pili ya mto ili wasimwone. Wakati wanafunzi wake walikuwa wamepanda chomboni na walikuwa wakikaribia ufukwe, walimwona Yesu akiwa anatembea juu ya maji. Petro alimwambia, “Bwana, niruhusu nije kwako.” Yesu akamjibu, “Njoo, kwa imani.” Petro akashuka kutoka chomboni na akaanza kutembea juu ya maji kuelekea Yesu. Hata hivyo, alipoanza kuhisi mashaka ndani yake, alianza kuzama. Ndipo Yesu akamshika mkono wake na kumwokoa

Kulisha watu 5000 mikate 5 na samaki 2.

Yesu alikuwa akiendelea kufundisha na umati mkubwa ulimwendea kumsikiliza. Wanafunzi wake waligundua kwamba muda ulikuwa umepita na watu hao hawakuwa wamekula. Kwa hiyo, wakamwambia Yesu, “Ruhusu watu hawa waende kijiji cha jirani kununua chakula.” Yesu akawajibu, “Wapeni ninyi chakula.” Wanafunzi wakasema, “Hatuna isipokuwa mikate mitano na samaki wawili.” Yesu akawaambia, “Waambieni watu waketi chini.” Kisha, akachukua mikate hiyo, akaibariki na kumshukuru Mungu, akachukua pia samaki, akafanya vivyo hivyo. Wanafunzi wakagawa mikate na samaki kwa watu, na kushangaza kwamba chakula hakikupungua, walishiba na hata zilisalia mabaki. Watu wote walishangaa na kustaajabu sana.

Kutoa fedha katika Mdomo wa samaki.

Wakati Yesu alipokuwa duniani, Israel ilikuwa chini ya utawala wa Kirumi, ambapo kodi ya kichwa ilikuwa ni sheria iliyotekelezwa. Siku moja, Petro alimwambia Yesu kwamba walihitaji kulipa kodi ya kichwa. Yesu akauliza, “Wafalme wa dunia hutoza kodi au ushuru kwa watu gani? Kwa watu wao au kwa wageni?” Petro akajibu, “Kwa wageni.” Yesu akamwambia, “Basi, ikiwa hivyo, wenyeji ni watu huru. Lakini tusije tukawakwaza. Nenda kwenye bahari, ukatupe ndoano, na samaki wa kwanza utakayemkamata, fungua kinywa chake, na utapata shekeli. Chukua hiyo na uwape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”

ISHARA YESU ALIZOZIFANYA KWA WATU.

Ni kweli, Yesu Kristo alifanya miujiza mingi juu ya watu, ambayo ilikuwa ya kushangaza sana na ilizidi kuimarisha imani ya watu kwake. Miujiza hiyo ilijumuisha mambo kama vile kuponya wagonjwa wasiojiweza, kuwatoa pepo wachafu kutoka kwa watu na pepo hao kumtii, kuponya vipofu, na hata kuwafufua wafu.

Hii ilisababisha watu wengi kuwa na mshangao na kuongeza imani yao kwake, na wengi wao waliamua kumfuata na kuyashuhudia matendo yake mwenyewe. Viongozi wa dini na wakuu wa watu, hata hivyo, walikuwa na upinzani na walimpinga. Walianza kujiuliza na kutafuta kujua mamlaka na nguvu gani ambayo Yesu alikuwa akiitumia kufanya mambo haya. Mjadala huu ulidumu kwa muda mrefu na ulisababisha viongozi wa dini kuchunguza na kutafuta mbinu za kumshitaki Yesu, na hata kupanga njama ya kumuua.

MAFUNDISHO YA YESU YALIYOJAA MAFUMBO.

Yesu alikuwa na njia ya kufundisha ambayo iliwashangaza watu wengi. Alitumia mifano na methali nyingi katika mafundisho yake, ambayo wengi hawakuelewa moja kwa moja. Maneno yake yalikuwa yamejaa hekima na waliyavuta watu kujihoji wenyewe na kujichunguza mioyoni mwao. Watu wengi walitubu na kuyashika maagizo na amri za Yesu, na wengine walistaajabishwa na busara na hekima ya maneno yake.

Kupitia mafundisho yake, Yesu aliwafundisha watu kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaonya juu ya njia zao za uovu na hila walizokuwa nazo mioyoni mwao. Hata hivyo, kwa njia ya mifano yake na maneno yake, baadhi ya Wayahudi walichukulia kama kufuru kwa Mungu. Walitafsiri maneno yake kama dharau kwa Mungu au kujifananisha naye. Hii ndiyo sababu baadhi yao walimshtaki na kumkemea Yesu kwa mafundisho yake.

  • Kusoma chuo cha Nabii Isaya na kuwaambia kwamba maneno hayo yametimia.

Yesu alipoingia katika sinagogi, alipewa kitabu cha Nabii Isaya ili asome. Baada ya kusoma sehemu ya unabii kutoka kitabu hicho, aliiambia jamii kwamba maneno hayo yametimia. Alimaanisha kwamba unabii huo ulikuwa unahusu maisha yake mwenyewe. Hata hivyo, watu waliposikia hilo, walimtoa nje ya sinagogi na kujaribu kumtupa katika bonde. Lakini Yesu alipita kati yao na akaenda zake, kwani wakati wake wa kutimiza kusudi lake ulikuwa bado haujafika.

  • Kumsamehe Kahaba dhambi.

Siku moja, Yesu alikuwa ameketi nyumbani kwa mwenyeji wake pamoja na wanafunzi wake na watu wengine. Wakati wa karamu, ghafla, mwanamke mwenye sifa ya kuwa kahaba alimkaribia Yesu, akajitupa miguuni mwake na kuanza kulia, akimfuta miguu yake kwa nywele zake. Watu waliohudhuria walishangaa na kusema kwamba kama Yesu angekuwa nabii, angejua kuwa mwanamke huyo alikuwa mwenye dhambi.

Lakini Yesu, ambaye alijua mawazo na nia za watu, akajibu kwa kumwambia mwenyeji wake, “Je, ulipoingiza nyumbani mwako hukunipa maji ya kunawa miguu wala taulo ya kujifuta? Lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kuisafisha kwa nywele zake. Kwa hiyo, dhambi zake zimesamehewa, kwa kuwa ameonyesha upendo na toba.” Kisha akamwambia yule kahaba, “Umesamehewa dhambi zako; nenda zako, na usitende dhambi tena.” Maneno haya yaliwafanya watu kushangaa na kujiuliza ni nani Yesu huyu anayeweza kusamehe dhambi za mtu?

  • Kusema kwamba Yeye ndiye Bwana wa sabato.

Wakati wa huduma yake, Yesu alimponya mwanamke aliyeteseka kutokwa na damu kwa miaka 12 siku ya sabato. Kwa mujibu wa sheria ya Israeli, ilikuwa marufuku kufanya matendo ya uponyaji siku hiyo. Watu wakamwuliza, “Kwa nini unafanya jambo hili siku ya sabato?” Yesu akawajibu, “Je, ninyi hamwezi kumwachia mnyama wenu atoke shimoni siku ya sabato? Basi vipi kuhusu huyu mwanamke, ambaye ni mwana wa Abrahamu, aliyeteseka kwa miaka 12? Sabato imeanzishwa kwa ajili ya binadamu, na si binadamu kwa ajili ya sabato.” Kwa maneno hayo, Yesu alijinena mwenyewe kuwa yeye ndiye Bwana wa sabato, akionyesha mamlaka yake juu ya sheria hiyo.

  • Kumwamuru mgonjwa aliyemponya kubeba godoro siku ya sabato.

Katika tukio hilo, Yesu alimponya mgonjwa kwenye birika la Siloamu, ambapo wagonjwa walikuwa wanasubiri maji kuguswa na malaika ili kuponywa. Baada ya kumponya, Yesu alimuambia mgonjwa huyo, “Simama, jitwike godoro lako na uende. Usitende dhambi tena, isije likakupata jambo baya zaidi.” Mtu huyo alisimama, akachukua godoro lake, na akaondoka.

Viongozi wa kidini walipomuona mgonjwa huyo akitoka na godoro lake siku ya sabato, wakamwuliza kwa nini anafanya hivyo, kwani ilikuwa ni marufuku kubeba vitu siku hiyo. Yule mgonjwa akawajibu kuwa yule aliyemponya alimwambia achukue godoro lake. Walitaka kujua ni nani aliyemwambia hivyo, lakini mgonjwa hakuweza kumtambua Yesu kwa sababu ya umati wa watu. Baadaye, alipomuona Yesu, alimwonesha wale viongozi wa kidini. Hii ilisababisha viongozi hao wamshitaki Yesu. Yesu aliwajibu viongozi hao akisema, “Baba yangu anaendelea kufanya kazi, na mimi ninaendelea kufanya kazi.” Kwa maneno hayo, Yesu alidhihirisha mamlaka yake ya kufanya kazi za Mungu, hata kwenye siku ya sabato.

  • Kumuita Mungu Baba yake.

Kwa kweli, katika mafundisho yake, Yesu alitumia neno “Baba” kumwita Mungu. Hii ilikuwa ni jambo jipya na la kipekee kwa Wayahudi wakati huo, ambao walikuwa na desturi ya kumtambua Mungu kwa majina mengine kama YHWH au Adonai. Kutumia neno “Baba” kumwita Mungu ilikuwa ni ishara ya uhusiano wa karibu na wa kipekee kati ya Yesu na Mungu.

Kwa Wayahudi wa wakati huo, kumwita Mungu “Baba” kulionekana kama kufuru au kutokuwa na heshima kwa Mungu. Waliona kuwa neno hilo lilikuwa linajihusisha na uhusiano wa kifamilia na Mungu, ambao waliamini ulikuwa ni wa pekee kwa taifa lao la Israeli. Hivyo, matumizi ya Yesu ya neno “Baba” kumwita Mungu yalizua utata na upinzani miongoni mwa viongozi wa kidini na baadhi ya Wayahudi.

Hata hivyo, Yesu alitumia neno “Baba” kwa umakini na kwa ufahamu kamili wa uhusiano wake wa karibu na Mungu. Alidai kuwa yeye ni Mwana wa Mungu na kwamba yeye na Baba yake ni kitu kimoja. Kwa njia hii, Yesu alijitambulisha kama Mungu mwenyewe na kuonesha uhusiano wake wa kipekee na Mungu. Hii ilikuwa moja ya mafundisho muhimu ya Yesu ambayo iliwashangaza na kuwakasirisha viongozi wa kidini wa wakati huo.

  • Kujiita kwa jina la Mungu “Mimi Nipo”.

Maneno “Mimi Nipo” (I AM) ambayo Yesu alitumia ni ya kipekee na yenye umuhimu mkubwa. Alikuwa akijitambulisha kwa jina hilo ambalo lilikuwa linahusishwa na Mungu katika Agano la Kale. Maneno hayo yalitumiwa na Mungu mwenyewe kumtambulisha Yeye mwenyewe kwa Musa wakati wa tukio la kichaka kibusha (bush) kule jangwani.

Kwa kusema “Kabla ya Ibrahimu kuwako, Mimi Nipo,” Yesu alikuwa anadai kuwa yeye alikuwepo kabla ya Ibrahimu, hivyo kudhihirisha kuwepo kwake tangu mwanzo na uungu wake. Hii ilikuwa ni madai makubwa ambayo yalimaanisha kwamba Yesu alikuwa Mungu mwenyewe, na hivyo kujitwalia hadhi sawa na ile ya Mungu. Wayahudi wa wakati huo waliitafsiri kauli hii kama kufuru kubwa, kwa sababu waliona ni kosa kwa mwanadamu kujitwalia cheo na jina la Mungu.

Watu waliojaribu kumpiga Yesu kwa mawe waliona kuwa alikuwa anajifanya sawa na Mungu na kukiuka heshima na ukuu wa Mungu. Hata hivyo, Yesu alitumia maneno haya kwa ufahamu kamili wa umoja wake na Baba yake wa mbinguni. Kwa kutumia jina hilo, alidai uungu wake na kueleza uhusiano wake wa kipekee na Mungu.

Ni muhimu kuelewa kwamba katika muktadha wa maandiko hayo, maneno ya Yesu hayakuwa tu kauli za kibinadamu, bali yalikuwa madai ya kiungu ambayo yalikuwa na lengo la kuwafunua watu ukweli juu ya utambulisho wake wa kimungu.

  • Kujitabiria Muda wa kufa na aina ya Kifo na Kufufuka.

Yesu alikuwa ametabiri muda wa kufa kwake, aina ya kifo chake, na ufufuko wake baada ya siku tatu. Alitabiri haya mara kadhaa kwa wanafunzi wake kabla ya kufa kwake.

Katika Mathayo 16:21, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba atateswa, atauawa, na atafufuka siku ya tatu. Pia, katika Mathayo 17:22-23 na Mathayo 20:17-19, alitoa unabii kuhusu mateso yake, kifo chake, na ufufuko wake.

Maneno haya ya unabii yalikuwa muhimu sana kwa imani ya wanafunzi wake na kwa ujumbe wa ukombozi ambao Yesu alikuwa akileta. Kwa kufufuka kwake kama alivyotabiri, imani yao ilithibitishwa na nguvu ya ufufuo wake ilikuwa msingi wa imani ya Ukristo.

Kwa hiyo, Yesu alikuwa ametabiri kwa ufasaha kabisa kuhusu kifo chake na ufufuko wake, na uthibitisho wa kutimia kwa maneno yake uliimarisha imani ya wanafunzi wake na wafuasi wengine baada ya ufufuko wake.

  • Kutoa amri mpya.

Katika Israeli, kulikuwa na desturi ya kuwepo kwa Manabii ambao watu waliwatumia kuuliza mambo kutoka kwa Mungu. Wakati Yesu alipokuwa hai duniani, kulikuwa na waandishi na viongozi wa kidini ambao walitoa tafsiri tofauti kuhusu amri za Mungu. Wakati Yesu alipokuwa akifundisha watu, walimfuata na kumuuliza jinsi ya kuelewa na kutafsiri maagizo na sheria za Mungu. Walipomuuliza kuhusu amri iliyo kuu zaidi, Yesu aliwajibu kwa kusema…

“Umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili yako yote. Amri nyingine kuu ni hii: Umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Kwa njia hii, amri nyingine zote zinatekelezwa. Kwa Waisraeli, inaweza kuonekana kana kwamba Yesu alikuwa akileta amri mpya ambazo hawakuwa wamepokea kutoka kwa Mungu.

  • Kusema Yeye ndiye atakayehukumu Ulimwengu.

Kwa mujibu wa imani ya Wayahudi, walikuwa na imani moja tu - kumwamini Mungu pekee na manabii ambao Mungu aliwatuma kwa jina Lake, ingawa wengi wa manabii hao walipoteza maisha yao kwa mikono ya watu wa Israeli. Kwa hiyo, katika imani yao, wanaamini kwamba ni Mungu pekee ndiye atakayehukumu ulimwengu siku ya mwisho. Wanafahamu kwamba Baba ameweka vyote mikononi mwa Mwana na Mwana anawagawia wale wote wanaompenda. Wanafahamu pia kwamba Mwana huyo ndiye atakayeamua mambo ya nyumba ya Israeli.

  • Yesu hakuwahi kusema nimezaliwa bali alisema nimekuja.

katika mazungumzo ya Yesu na wanafunzi wake na pia katika hotuba zake kwa umma, hakutumia mara kwa mara maneno “nimezaliwa”, bali alitumia mara kwa mara maneno “nimekuja”. Hii inaonyesha ufahamu wake wa asili yake na utume wake. Alitambua kwamba yeye alikuwa amekuja kutoka mahali fulani ambapo sisi hatujui, na hivyo alitumia maneno hayo kuwasilisha ukweli huo. Hii inaonyesha kwamba alikuwa na ujuzi na ufahamu wa kipekee juu ya asili yake na kusudi lake katika kuwepo kwake duniani.

  • Utakatifu wa Yesu.

Utakatifu wa Yesu ni jambo lenye upekee sana. Hata wale ambao walimpinga na kumchukia, kama vile viongozi wa Kiyahudi ambao walikuwa wakitafuta kumshitaki kwa makusudi, hawakuweza kupata kosa lolote la kumshitaki. Hii inaonyesha kwamba Yesu aliishi maisha ya haki na utakatifu ambayo hayakuwa na hatia. Tangu mwanzo wa huduma yake, Yesu alionyesha ukamilifu na usafi wa kiroho. Alikuwa mtu ambaye aliishi kikamilifu kulingana na mapenzi ya Mungu na akafuata sheria za kimungu kwa ukamilifu. Hata katika mazingira ya upinzani na majaribu, Yesu hakufanya dhambi au kukiuka maadili ya Mungu.

Utakatifu wa Yesu unaonyesha asili yake ya kimungu na pia uaminifu wake kwa Baba yake wa mbinguni. Alikuwa bila doa na mwenye haki, na hii ilithibitishwa na watu wengi waliomzunguka, hata wale ambao walikuwa na nia mbaya dhidi yake. Utakatifu wa Yesu unathibitisha kwamba yeye ni Masihi mwenye haki na kamili, aliyetumwa na Mungu kuwaokoa watu na kuwaletea wokovu. Utakatifu wake unatuongoza na kutuhamasisha kuishi maisha ya utakatifu na kuiga mfano wake.

USHUHUDA WA YESU.

Ushuhuda wa Yohana Mbatizaji.

Yesu alishuhudiwa kwanza na Yohana mbatizaji, kisha akashuhudiwa na Mbingu kwa njia ya Roho mtakatifu, kisha baadae wanafunzi wake wenyewe ya kwamba ndiye Kristo ambaye kupitie yeye Israeli na ulimwengu utakombolewa kutoka katika dhambi zao. Lakini yesu mwenyewe alisema na watu hao akiwaambia, mimi sishuhudiwi kwa ushuhuda wa mwanadamu bali Baba yangu aliyenituma ndiye anishuhudiaye kupitia hizo kazi nizifanyazo kwenu, ambazo hakuna mtu aliyewahi kuzifanya hapo kabla, Kama hamniamini mimi basi ziaminini hizo kazi nizifanyazo.

Ushuhuda wa Nikodemu.

Ni kweli kwamba umetoka kwa Mungu, maana hakuna awezaye kutenda yote uyatendayo kama Mungu hayupo pamoja naye. Maneno haya ni maneno ya NIKODEMU ambaye alikuwa mkuu wa mwalimu wa dini ya wayahudi. akusema kwamba alizitenda kazi zilizokuwa zinadhihirisha utukufu wa Mungu na sio utukufu wake, kitendo hichi ni kusema kwamba Yesu alifunika utukufu wake na kumuinua Mungu atukuke zaidi ili MUNGU NAYE AMUINUE YEYE.

Mwalimu mwema

Mafundisho ya Yesu Kristo yalibeba wema wa kimungu ndani yake, kiasi kwamba hata wanafunzi na makutano walipokuwa wakiyasikia walistajaabu mara kadhaa wakitafakari hekima ya Mungu pamoja na mamlaka aliyokuwa nayo Yesu Kristo hata mapepo na nguvu zingine kutiishwa kwa mamlaka hiyo.


Stay in touch

If you enjoyed this post, then don't miss out on any future posts by subscribing to my email newsletter

Support my work by sharing the link or by contact through +255 768 596 017.

Share