Tafsiri Potofu: Jinsi huduma takatifu zimegeuzwa kuwa sanamu.
Ni muhimu sana kuweka imani na shukrani zetu kwa Mungu mmoja kwa sababu ya upendo wake kwetu. Tumebarikiwa kwa kujitoa kwake Yesu Kristo, ambaye alikuwa sadaka ya upatanisho kati yetu na Mungu kwa ajili ya dhambi zetu. Kupitia imani yetu katika Yesu Kristo, sisi sote tumejaliwa kuwa watoto wa Mungu na kupewa uwezo wa kuishi maisha takatifu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuishi kulingana na mapenzi ya Mungu na si kuongozwa na maarifa ya kibinadamu kuhusu mambo ya kiroho. kuna baadhi ya tafsiri potofu ambazo zimeenea na kuaminiwa na watu wengi, lakini Mungu anaziona kama ibada za sanamu, machukizo, na makufuru mabaya.

Kwa kufanya vitu hivyo kuwa sehemu ya ibada, watu wamepoteza umuhimu wa kujitoa wenyewe katika kumwabudu Mungu kwa njia ya kweli. Watu wengi wanadai kuwa waumini wa kweli, lakini swali la kujiuliza ni, “Je, unaamini imani ipi? Je, ni imani iliyotokana na Mungu au imani iliyotokana na mafundisho ya wanadamu?”
Huduma takatifu zilizopotoshwa na tafsiri za dini:
- Fundisho la ubatizo wa maji kama ishara ya kuzaliwa mara ya pili (wokovu).
- Kuongoza/kuongozwa katika sala ya toba.
- Biblia kufanywa kiongozi kwa Wakristo.
- Mafundisho ya sadaka za ukombozi, ili kufutwa kwa laana za ukoo na mikosi, na kupata baraka.
- Kuamini nguvu za Mungu kupitia ishara za miujiza pekee bila kuishi maisha ya utakatifu.
Ni muhimu kutambua kwamba hizi ni tafsiri potofu ambazo zimezoeleka, lakini siyo sehemu ya ibada ya kweli mbele za Mungu. Tunapaswa kuwa waangalifu na kufuata mafundisho ya Mungu yaliyoandikwa katika Neno lake, Biblia, na kuongozwa na Roho Mtakatifu katika kumwabudu Mungu kwa njia inayompendeza.
Madhabahu
Katika majengo ya makanisa niliyoyazungumzia hapo awali, ni kawaida kukuta mahala fulani mbele ya jengo hilo, pameandaliwa na pamewekwa tofauti kabisa na eneo lingine ambapo makutano wanakaa. Hiyo ni kutokana na umuhimu wa eneo hilo katika tafsiri yetu ya kibinadamu, eneo hilo hupambwa kwa vitambaa na rangi mbalimbali, nyingine zikiwa zinabeba maana fulani na nyingine ikiwa ni kuleta muonekano mzuri wenye kupendeza machoni. Sio ajabu kwa nyakati hizi unaweza ukaona jengo ambalo halijakwisha vizuri ujenzi ila ukiingia ndani ya jengo hilo liitwalo Kanisa, ukakuta pamepambwa tofauti na uhalisia wa jengo.
Ukweli ni kwamba ni eneo linaloheshimika zaidi katika jengo lote la kanisa, wengine wakipita mbele yake huina na kutoa ishara ya heshima,na wengine husujudu kama kuashiria utakatifu wa eneo hilo,na wengine hawawezi hata kuthubutu kupakanyaga kwa miguu yao wenyewe kwa hofu ya utakatifu wa eneo hilo.
Kwanza tutafute Neno madhabahu limeanzia wapi na ilikuwa kwa ajili ya nini,na lilibeba maana gani nyuma yake. Mwanzo 8: 20, Mwanzo 12:7. Tunaona madhabahu ilikuwa ni eneo la kumtolea Bwana Mungu sadaka ya Kuteketeza,ikiwa ni wanyama au mazao,na vilikuwa vinateketezwa vingali hai.hivyo ndivyo madhabahu ilivyokua inajengwa na kufanya kazi ya kumtolea Bwana Mungu sadaka za kuteketezwa.
- Je, ni kweli kwamba katika dunia inaweza kuwepo eneo ambalo linathaminiwa zaidi kuliko Mungu?
- Je, kama Mungu anaishi ndani ya watu kupitia Yesu Kristo, je, kuna uwezekano wa kuwa na eneo katika - kanisa lenye heshima zaidi kuliko mtu aliye na Mungu ndani yake?
- Kati ya mwanadamu na vitu vyote katika dunia, ni kipi kinachopewa umuhimu zaidi?
- Je, ni sahihi kuonyesha heshima kwa watu wacha Mungu au kutukuza eneo lililopo madhabahuni?
- Je, Mungu anakaa ndani ya watu au anakaa katika majengo?
- Kwa nini tunatukuza maeneo dhaifu na vitu vya kidunia kwa utukufu ambao hatuwapi watu ambao Kristo Yesu anaishi ndani yao?
Shukrani.
Shukrani ni miongoni mwa mambo yanayochanganywa na uhalisia wake katika mafundisho ya kidini. Elimu inayosambaa kuhusu shukrani ni kwamba tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kile anachotupatia katika malengo yetu au kazi tunazofanya. Ni kweli kwamba Mungu anabariki kazi zetu zilizofanywa kwa haki na bila dhuluma, lakini tunapaswa kumshukuru kwa kila jambo, si tu kwa yale ambayo tumeyaweka malengo na yametimia. Aidha, kumshukuru Mungu kwa jambo maalum kunamnyima Mungu utukufu, kwani afya na uhai pekee ni jambo ambalo tunapaswa kumshukuru kwa ajili yake.
Badala ya kumshukuru Mungu kwa mambo maalum, tunapaswa kumshukuru kwa kila jambo, wakati wote na mahali popote, kwa sababu kuwa hai na kuona siku na saa zinapoendelea, iwe kuna changamoto au faraja, ni neema ya Mungu. Ikiwa tutazidi kumshukuru Mungu kwa kuzingatia baraka zake za kimwili, tutapoteza lengo la utukufu wa Mungu katika roho. Shukrani ya kweli mbele za Mungu ni matendo mema na maisha ya kumtegemea Yesu Kristo, ambayo yanatambua upendo wake na msamaha wake wa dhambi zetu kupitia kifo cha Yesu Kristo. (Warumi 12:1)
Fungu la kumi.
Mwanzo 14:20kwa mara ya kwanza neno FUNGU LA KUMI, Abrahimu akimpa Mfalme wa selemu Melkizedeki sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyoviteka kutoka katika sehemu za hao adui zake aliowashinda katika vita. Mungu hakumpa Amri Abrahamu kutoa Fungu la kumi kwa Melkizedeki, bali baada ya Melkizedeki kutoka kwenda kumlaki Abrahamu baada ya kushinda vita. Melkizedeki alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana, Ndipo Abrahamu aliamua kumpa sehemu ya kumi ya mali alizozitwaa kwa maadui zake. Kumbukumbu la Torati 14:22 – 29. Katika kitabu hiki tunaona namna ambavyo fungu la kumi linageuzwa kutoka kuwa hiyari na kufanywa kuwa sheria. Ikisema, “Utatoa sehemu ya kumi ya maongeo yako na wanyama na divai na mafuta, mwaka kwa mwaka.” Lakini inaenda mbele zaidi na kuonesha namna unavyopaswa kutolewa na jinsi ya kutumika kwake.
Fungu la kumi, au zaka, ni aina ya sadaka ambayo ina historia na utaratibu wake katika Agano la Kale. Mungu aliwaamuru wana wa Israeli kutoa sehemu ya kumi ya mali zao, iwe ni wanyama au mazao, kama sadaka kwa ajili ya utumishi wa kidini. Wana wa Israeli walikuwa wafugaji na wakulima, na hivyo walitakiwa kutoa sehemu ya kumi ya mazao yao ya shamba na mifugo yao kama sehemu ya kumtumikia Mungu. Fungu la kumi lilikuwa na utaratibu maalum wa kutolewa na matumizi yake. Wana wa Israeli walikuwa wanakusanya mazao yao na kuchagua sehemu ya kumi ya mazao hayo kama fungu la kumi. Fungu hilo la kumi lilitolewa kwa makuhani na Walawi, ambao walikuwa waaminifu katika huduma ya kidini. Walawi nao walitoa sehemu ya kumi ya fungu hilo la kumi kama sadaka kwa Bwana.
Fungu la kumi lilitumiwa kwa ajili ya kusaidia huduma za kidini na kusaidia makuhani na Walawi ambao hawakuwa na urithi wa ardhi na walitegemea sadaka za watu kwa ajili ya mahitaji yao. Pia, fungu la kumi lilitumiwa kwa ajili ya kusaidia maskini, mayatima, na wageni ambao walikuwa hawana uwezo wa kujitegemea. Lengo la fungu la kumi lilikuwa kuonyesha utii na kutambua kwamba mali zote ni za Mungu na tunapaswa kumtumikia kwa moyo wa ukarimu. Pia, ilikuwa njia ya kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii ya Israeli kwa kugawana rasilimali na kusaidia wale waliohitaji.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba Agano la Kale na taratibu zake za kidini zilikuwa sehemu ya uhusiano maalum kati ya Mungu na taifa la Israeli katika wakati huo. Katika Agano Jipya, taratibu nyingi za Agano la Kale zimefikia ukamilifu wake katika kazi ya Yesu Kristo, na tunajielekeza zaidi katika kanuni za upendo, ukarimu, na huduma kwa wengine.
(Kufuatia hayo nashawishika kusema kwamba Abrahamu alikuwa mcha Mungu na alikuwa mnyofu mbele ya Mungu, hivyo yawezekana alipata muongozo wa Mungu kabla ya kulifanya jambo hilo.Au kwakuwa Mungu alikuwa kiongozi wake basi Alimpa hekima ya kufanya jambo jema lenye kumpendeza Mungu.) hayo ni mawazo yangu sio maandiko yasemavyo.
Fungu la kumi kwa Wayahudi.
Torati iliagiza kwamba, ukishakuvitoa hivyo vitu vya fungu la kumi, utakula wewe uliyevitoa na familia yako na mlawi aliyeko katika nyumba yako kwa maana mlawi hakupewa sehemu katika Israeli bali alikuwa ni kuhani wa Mungu. Taratibu hii iliendelea hata wakati Yesu alipokuja alikuta utaratibu huo unadumishwa na mambo mengine yaliongezeka, kwa mujibu wa maandiko katika kitabu cha Yohana, siku moja Yesu alikwenda hekaluni akakuta watu wamegeuza sehemu ya hekalu kuwa soko. akapindua meza na kuwafungulia mifugo na njiwa akisema “Nyumba ya Baba yangu iliwekwa kuwa nyumba ya ibada, ninyi mmeigeuza kuwa soko”. Hayo yalikuwa mwisho wa mwaka kwa Israeli na walikuwa wakikutana Yerusalemu kwa ajili ya kumwadhimisha Bwana Mungu na kutoa zaka na sadaka za maondoleo ya dhambi pamoja na sadaka nyingine.
Utaratibu ulielekeza, baada ya mwaka wa tatu, mtoaji wa fungu la kumi aitende sadaka hiyo na kuiweka ndani mwake, yaani hatapeleka mahala pa makutano bali atakula yeye na watu wa nyumbani mwake na mgeni na mjane na yatima na mlawi kwa maana hakupewa sehemu katika Israeli. Na maandiko yanasema imempasa mtoaji wa fungu la kumi kufanya hivyo ili kusudi ajifunze kumcha Bwana Mungu na ndipo Mungu ataibariki kazi ya mikono yako.

Fungu la Kumi katika Agano Jipya.
Ili kulijenga swali letu, ni vyema tukaangalia ni kwa namna gani hao Mitume wa kwanza katika Imani yetu kwa Yesu Kristo, walivyofanya taratibu katika matoleo (Sadaka) kwenye makutano/walipokusanyika, je. Fungu la kumi lilikuwepo katika matoleo yao?, Matendo ya Mitume 4: 31 – 37 na Matendo ya Mitume 5: 1 – 14. Katika mistari hiyo tunaona kwamba hao waamini wa kwanza wa Imani kwa Yesu Kristo, walikuwa wakikusanyika pamoja kama familia moja, na kila mmoja alileta vitu vyake vyote miguuni pa Mitume, nao Mitume wakawagawia watu kulingana na mahitaji yao, na maandiko yanaonesha hapakuwa na mtu asiyetimiziwa uhitaji wake kwa sababu waligawiwa kulingana na mahitaji ya Mtu.
Je, halali kwa Mkristo kutoa fungu la kumi? Swali limekuwa na mitazamo tofauti katika jumuiya za Kikristo. Kuna wale ambao wanafuata desturi ya Agano la Kale na kuendelea kutoa fungu la kumi kama sehemu ya ibada yao, na kuna wengine ambao hawatoi fungu la kumi kwa msingi kwamba mafundisho ya Agano la Kale yamepita na yamebadilishwa na Agano Jipya.
Kwa upande wa wale wanaoendelea kutoa fungu la kumi, msingi wao ni kwamba mafundisho ya Agano la Kale hayajabadilika na kwamba wanaendelea kumtii Mungu kwa njia hiyo. Wanaweza kuona mfano katika Maandiko kama vile Malaki 3:10, ambapo Mungu anawaambia watu wake “Toeni fungu kamili katika nyumba yangu… nijaribuni kwa njia hii, asema Bwana wa majeshi, kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, ili mpate kula” (Malaki 3:10).
Kwa upande wa wale ambao hawatoi fungu la kumi, msingi wao unategemea mabadiliko yaliyotokea katika Agano Jipya. Wanasisitiza kuwa tunaishi chini ya neema ya Yesu Kristo na kwamba tunapaswa kutoa kwa moyo wa ukarimu na kusaidia wengine kulingana na uwezo wetu na kwa utambuzi wa Roho Mtakatifu. “Tukisema ni halali tutakuwa tunajidanganya wenyewe, kwa sababu maandiko yatatupinga na kwamba tutakwenda kinyume na kusanyiko la kwanza la Mitume waliokuwa Mashuhuda wa ile Nuru. Ambao ndiyo waasisi wa Imani katika Kristo Yesu.” Rejea……*Waebrania 7: 1 – 28/ Waebrania 8: 1 – 13.
Ni muhimu kukumbuka kuwa maamuzi haya ya kutoa au kutokutoa fungu la kumi ni masuala ya kibinafsi na yanapaswa kuongozwa na dhamiri ya mtu binafsi na uelewa wa Neno la Mungu. Kila Mkristo anapaswa kuchunguza Maandiko, kusali, na kutafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu katika kufanya maamuzi kuhusu kutoa na jinsi ya kutoa kwa ajili ya kazi ya Mungu na huduma ya wengine. Tunapaswa kuwa na moyo wa ukarimu, kuwajali wengine, na kutumia rasilimali zetu kwa hekima na kulingana na mwongozo wa Mungu.

Sala ya toba.**
Sala ya toba imekuwa ni kama kanuni ya kwanza kwa muamini mpya katika kumjua Yesu Kristo, sala hii inaendelea kupata umaarufu mkubwa na kuonekana kana kwamba ni utaratibu sahihi wa kumwendea Yesu Kristo. kinyume na mafundisho ya Mitume Efeso 2: 1 – 10, Warumi11: 1 – 6, Warumi 3: 24, Tito 3: 3 – 10. Wokovu wa matendo ni mtego wa sgetani kwa waamini wa Yesu Kristo. Ndio maana unaweza kumkuta mtu anasema nina miaka kadha wa kadha katika wokovu. Hii ni kwa sababu ni jambo aliloliratibu na kuliamua yeye mwenyewe, wala sio tena uweza wa Mungu kwa Msaada wa Roho Mtakatifu. Yesu akamwambia Nikodemu, “Je, unaweza kuona upepo unapovuna unaanzia wapi au unakwenda wapi?, lah! hasha bali unauhisi, vivyo hivyo azaliwaye Rohoni hana mwazo wake wala mwisho.” maana yake ni kwamba, hakuna mwanzo wa kusema leo au kesho au jana nilizaliwa Rohoni (Mara ya pili) bali utakacho kihisi ni uweza wa Mungu kwa nguvu za Roho mtakatifu atakayejazwa ndani yako).
Kunena kwa lugha.**
Moja ya kituko na ulaghai uliojipenyeza katika fundisho la leo katika mikusanyiko na pia mikutano ya Imani ya Kikristo, ni kuwafundisha watu namna (style) za kuwawezesha kunena kwa lugha. fundisho hili sio kificho wala aibu tena bali imekuwa jambo la kimkakati kuwafanya watu waamini wamejazwa Roho Mtakatifu. Maandiko yanasema “Mitume walipojazwa Roho Mtakatifu wakaanza kila mmoja kunena kwa lugha mpya asiyoijua”, na hata wale walioamini baadaa ya hao mitume kuwahubiria wakajazwa Roho mtakatifu na kuanza kunena kwa lugha mpya. Hakuna mahala Biblia imefundisha au kuandika kwamba yupo mtume au nabii au mwalimu alifika akawahubiria watu habari za Yesu Kristo kisha walipoamini akawafundisha kunena kwa lugha. Kwa sababu kunena kwa lugha ni karama mtu anayopewa kutoka kwa Mungu, kama ishara mojawapo ya nguvu za Mungu, na ishara za kujzwa Roho Mtakatifu zipo nyingi sio ya Kunena Kwa lugha pekee. Hivyo mtu anapojaribu kumfundisha mwingine kunena kwa lugha ni kuchukua utkufu wa Mungu kuwa utukufu wake mwenyewe.
Mathayo: 7: 12 – 24
Basi ye yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo, maana hiyo ndiyo torati na manabii. Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba, maana mlango ni mpana, na njia ni pana ieleayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba na njia imesonga iendayo uzimani nao waionao ni wachache. Jihadharini na manabii wa uongo watu wawajiao wamevaa mavazi ya Kondoo,walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.Mtawatambua kwa matunda yao,je,watu huchuma zababibu katika miiba,au tini katika mibaruti?.Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri,na mti muovu huzaa matunda mabaya.Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya,wala mti muovu kuzaa matunda mazuri.Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa ukatupwa motoni.Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. Si kila mtu aniambaiye Bwana Bwana ataingia katika ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye Mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana hatukufanya miujiza kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?. Ndipo niwaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe, ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu. Basi kila asikaye hayo maneno yangu na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.